Yesu Abadilika Sura Mlimani

17 Baada ya siku sita, Yesu akawachukua Petro, Yakobo na Yohana ndugu yake Yakobo, wakaenda peke yao juu ya mlima mrefu. Na wakiwa huko, Yesu akabadilika sura mbele yao, uso wake ukang’aa kama jua na nguo zake zikawa nyeupe kama mwanga. Na mara Musa na Eliya wakawatokea, wakawa wakizungumza na Yesu. Kisha Petro akamwambia Yesu, “Bwana, ni vizuri kwamba sisi tuko hapa. Ukiniruhusu, nitatengeneza vibanda vitatu hapa: kimoja chako, kingine cha Musa na kingine cha Eliya.”

Petro alipokuwa bado akizungumza, ghafla, wingu linalong’aa likatanda juu yao na sauti ikatoka kwenye wingu hilo ikasema, “Huyu ni mwanangu mpendwa, ambaye nimependezwa naye; msikilizeni yeye.” Wanafunzi waliposikia haya walianguka chini kifudifudi wakajawa na hofu. Lakini Yesu akaja, akawagusa, akawaambia, “Inukeni. Msiogope.” Walipoinua macho yao hawakumwona mtu mwingine isipokuwa Yesu peke yake.

Walipokuwa wakishuka mlimani, Yesu akawaambia, “Msimwambie mtu ye yote maono haya mpaka mimi Mwana wa Adamu nitakapofufuliwa kutoka kwa wafu.”

Read full chapter