Yesu Ni Bwana Wa Sabato

12 Wakati huo Yesu alipitia kwenye mashamba ya ngano siku ya sabato. Wanafunzi wake walikuwa na njaa, wakaanza kuvunja masuke ya ngano na kula. Lakini Mafarisayo walipoona jambo hili wakam wambia, “Tazama! Wanafunzi wako wanafanya jambo lisilo halali kufanya siku ya sabato.”

Yesu akawajibu, “Hamjasoma walichofanya Daudi na wafuasi wake walipokuwa na njaa? Waliingia katika nyumba ya Mungu wakala mkate uliowekwa wakfu, jambo ambalo halikuwa halali kwao kufanya isipokuwa makuhani peke yao. Au hamjasoma katika sheria kwamba siku ya sabato makuhani huvunja sheria ya sabato Hekaluni lakini hawahesabiwi kuwa na hatia? Nawaambieni wazi kwamba, aliye mkuu kuliko Hekalu yupo hapa. Na kama mngalifahamu maana ya maneno haya, ‘Ninataka rehema wala si sadaka ya kuteketezwa;’ msingeliwalaumu watu wasio na hatia, kwa maana Mwana wa Adamu ni Bwana wa sabato.”

Read full chapter