Yesu Awaonya Mafarisayo Na Wanasheria

37 Yesu alipomaliza kuzungumza, Farisayo mmoja alimkaribisha nyumbani kwake kwa chakula. Yesu akaingia na kuketi chakulani moja kwa moja. 38 Farisayo yule alipoona kwamba Yesu hakunawa kwanza kabla ya kula alishangaa. 39 Ndipo Bwana akamwambia, “Ninyi Mafarisayo mnasafisha kikombe na sahani kwa nje huku ndani mmejaa udhalimu na uovu. 40 Wajinga Ninyi! Hamjui kuwa yeye aliyetengeneza sehemu ya nje ndiye aliyetengeneza na ya ndani pia? 41 Watendeeni ukarimu maskini kwa kuwapa vilivyomo ndani ya vikombe na sahani zenu na kila kitu kitakuwa safi kwenu.

42 “Lakini ole wenu, Mafarisayo! Ninyi mnamtolea Mungu sehemu ya kumi ya mnanaa, mchicha na kila aina ya mboga lakini mnapuuza haki na kumpenda Mungu. Mngeweza kutoa matoleo hayo pasipo kusahau haki na upendo kwa Mungu.

43 “Ole wenu, Mafarisayo! Ninyi mnapenda kuketi viti vya mbele katika masinagogi na kusalimiwa kwa heshima masokoni! 44 Ole wenu! Kwa maana ninyi ni kama makaburi yasiyokuwa na alama, ambayo watu huyakanyaga pasipo kujua.”

45 Mwalimu mmoja wa sheria akasema, “Mwalimu, unapozungumza hivyo unatushutumu na sisi wanasheria!” 46 Yesu akamjibu, “Hata ninyi wanasheria, ole wenu! Mnawabebesha watu mzigo wa sheria ambazo hawawezi kuzitimiza; wala hamfanyi lo lote kuwa saidia iwe rahisi kwao kuzitimiza. 47 Ole wenu kwa kuwa mnawa jengea makaburi manabii waliouawa na babu zenu. 48 Kwa kufanya hivyo mnakiri kwamba mnaunga mkono kitendo hicho walichofanya babu zenu. Wao waliua na ninyi mnatengeneza makaburi.

49 “Ndio maana Mungu katika hekima yake alisema, ‘Nita wapeleka manabii na mitume, na baadhi yao watawaua na wengine watawatesa.’ 50 Kwa hiyo damu ya manabii wote iliyomwagika tangu mwanzo wa dunia itahesabiwa juu ya watu wa kizazi hiki; 51 tangu damu ya Abeli mpaka damu ya Zakaria aliyeuawa kati ya madhabahu na mahali patakatifu. Nawaambia kweli, watu wa kizazi hiki wataadhibiwa kwa ajili yao wote. 52 Ole wenu ninyi wanashe ria kwa maana mmeuchukua ufunguo unaofungua nyumba ya maarifa. Ninyi wenyewe hamkuingia na wale waliokuwa wanaingia mkawazuia.”

53 Yesu alipoondoka hapo, walimu wa sheria na Mafarisayo wakawa wanampinga vikali na kumwuliza maswali mengi, 54 wakijar ibu kumtega ili aseme kitu ambacho watakitumia kumshitaki.

Read full chapter

Yesu Awakosoa Viongozi wa Kidini

(Mt 23:1-36; Mk 12:38-40; Lk 20:45-47)

37 Baada ya Yesu kumaliza kuzungumza, Farisayo mmoja alimwalika Yesu kula pamoja naye. Hivyo Yesu alikwenda na kuketi sehemu ya kulia chakula. 38 Lakini Farisayo alishangaa alipoona Yesu hakunawa[a] mikono yake kwanza kabla ya kuanza kula. 39 Bwana akamwambia, “Usafi mnaoufanya ninyi Mafarisayo ni kama kusafisha kikombe au sahani kwa nje tu. Lakini ndani yenu mna nini? Mnataka kuwadanganya na kuwaumiza watu tu. 40 Ninyi ni wajinga! Aliyeumba kilicho nje ndiye aliumba kilicho ndani. 41 Hivyo, jalini vilivyo ndani. Wapeni vitu wenye uhitaji. Ndipo mtakuwa wasafi kikamilifu.

42 Lakini, ole wenu ninyi Mafarisayo! Mnampa Mungu sehemu ya kumi ya vyakula mnavyopata, hata mnanaa, na hata kila mmea mdogo katika bustani[b] zenu. Lakini mnapuuzia kuwatendea haki wengine na kumpenda Mungu. Haya ni mambo mnayotakiwa kufanya. Na endeleeni kufanya mambo hayo mengine.

43 Ole wenu ninyi Mafarisayo, kwa sababu mnapenda kupata viti vya heshima katika masinagogi. Na mnapenda kusalimiwa na watu kwa kuheshimiwa sehemu za masoko. 44 Ole wenu, kwa kuwa mnafanana na makaburi ya zamani yasiyoonekana, ambayo watu hupita juu yake na kuyakanyaga bila kuyatambua.”

45 Mmoja wa wanasheria akamwambia Yesu, “Mwalimu, unaposema mambo haya kuhusu Mafarisayo unatukosoa hata sisi pia.”

46 Yesu akamjibu, “Ole wenu, enyi wanasheria! Mnatunga sheria kali ambazo ni vigumu watu kuzitii.[c] Mnawalazimisha wengine kuzitii sheria zenu. Lakini ninyi wenyewe hamthubutu hata kujaribu kufuata mojawapo ya sheria hizo. 47 Ole wenu kwa kuwa mnajenga makaburi ya manabii. Lakini hawa ni manabii wale wale ambao mababu zenu waliwaua. 48 Na sasa mnawaonesha watu wote kwamba mnakubaliana na mambo ambayo baba zenu walifanya. Waliwaua manabii, nanyi mnasherehekea mauaji hayo kwa kujenga makaburi ya manabii! 49 Hii ndiyo sababu ambayo kwa Hekima yake Mungu alisema, ‘Nitawatuma manabii na mitume[d] kwao. Baadhi ya manabii na mitume wangu watauawa na watu waovu. Wengine watateswa sana.’

50 Hivyo ninyi watu mnaoishi sasa mtaadhibiwa kwa sababu ya vifo vya manabii wote waliouawa tangu mwanzo wa ulimwengu. 51 Mtachukuliwa wenye hatia kutokana na vifo hivyo vyote, tangu kuuawa kwa Habili mpaka kuuawa kwa nabii Zakaria,[e] aliyeuawa kati ya madhabahu na Hekalu. Ndiyo ninawaambia, kizazi hiki kitaadhibiwa kwa sababu yao wote.

52 Ole wenu, ninyi wanasheria, mmechukua ufunguo wa kujifunza kuhusu Mungu. Ninyi wenyewe hamtaki kujifunza na mmewazuia wengine wasijifunze pia.”

53 Yesu alipotoka humo, walimu wa sheria na Mafarisayo walianza kumpinga sana. Walianza kumjaribu ili awajibu maswali kuhusu mambo mengi, 54 ili Yesu akisema jambo isivyo sahihi waweze kupata sababu ya kumkosoa.

Read full chapter

Footnotes

  1. 11:38 hakunawa Hakunawa kwa maana ya kuwa kunawa mikono au kuoga mwili wote ilikuwa desturi ya dini ya Kiyahudi na Mafarisayo waliipa desturi hii umuhimu mkubwa.
  2. 11:42 Mnampa … bustani Kwa maana ya kawaida, “Mnatoa zaka za mnanaa, mchicha na kila aina ya mboga mboga.” Sheria ya Musa iliwataka Waisraeli kushirikiana chakula kwa kutenga sehemu ya kumi ya mazao na mifugo yao kwa ajili ya Mungu (tazama Law 27:30-32; Kum 26:12). Hii haikujumuisha mazao madogo ya bustani kama yaliyotajwa hapa. Hivyo Mafarisayo hawa walikuwa wanatoa zaidi ya inavyotakiwa ili kuhakikisha kuwa hawavunji sheria.
  3. 11:46 Mnatunga sheria kali … watu kuzitii Kwa maana ya kawaida, “Mnawatwisha watu mizigo wasiyoweza kuibeba.”
  4. 11:49 manabii na mitume Watu waliochaguliwa na Mungu kuhubiri Habari Njema ulimwenguni.
  5. 11:51 Habili … Zakaria Katika Agano la Kale la Kiebrania, hawa ni watu wa kwanza na wa mwisho kuuawa. Tazama Mwa 4:8-11 na 2 Nya 24:20-25.