40 Kwa maana mapenzi ya Baba yangu ni haya: wote wamwonao Mwana na kumwamini wawe na uzima wa milele. Nami nitawafufua siku ya mwisho.”

41 Wayahudi wakaanza kunung’unika kwa kuwa alisema: “Mimi ni mkate ulioshuka kutoka mbinguni.” 42 Wakasema, “Huyu si Yesu mwana wa Yusufu? Na baba yake na mama yake si tunawajua? Anawezaje basi kutuambia kwamba ameshuka kutoka mbinguni?”

43 Lakini Yesu akawaambia, “Acheni kunung’unika. 44 Hakuna mtu awezaye kuja kwangu kama Baba aliyenituma hakumvuta kwangu; nami nitamfufua siku ya mwisho. 45 Kama manabii walivyoandika, ‘Wote watafundishwa na Mungu.’ Ye yote amsikilizaye Baba na kuji funza kutoka kwake, huja kwangu. 46 Hii haina maana kwamba kuna mtu aliyekwisha kumwona Baba. Ni yule aliyetoka kwa Mungu peke yake, ndiye aliyekwisha kumwona Baba. 47 Nawaambieni kweli: anayeamini anao uzima wa milele. 48 Mimi ni mkate wa uzima. 49 Baba zenu walikula mana jangwani, wakafa. 50 Lakini hapa kuna mkate utokao mbinguni ambao mtu ye yote akiula, hatakufa. 51 Mimi ni mkate wa uzima uliotoka mbinguni. Mtu ye yote akiula mkate huu ataishi milele. Na mkate wenyewe ni mwili wangu ambao nitautoa ili watu wote ulimwenguni wapate kuishi milele.”

52 Hapo Wayahudi wakaanza kubishana kwa hasira wakiulizana, “Mtu huyu awezaje kutupatia mwili wake tuule?”

53 Kwa hiyo Yesu akasema, “Ninawaambieni hakika, msipoula mwili wangu mimi Mwana wa Adamu na kuinywa damu yangu, hamtakuwa na uzima ndani yenu. 54 Mtu ye yote alaye mwili wangu na kunywa damu yangu anao uzima wa milele; nami nitamfufua siku ya mwisho. 55 Kwa maana mwili wangu ni chakula halisi na damu yangu ni kinywaji halisi. 56 Ye yote alaye mwili wangu na kunywa damu yangu anaishi ndani yangu na mimi ninaishi ndani yake.

Read full chapter