Petro Amfufua Dorkasi

36 Huko Jopa kulikuwa na mwanafunzi mwanamke aliyeitwa Tabita au kwa lugha ya Kigiriki, Dorkasi, yaani paa. Huyu mama alikuwa mkarimu sana, akitenda mema na kuwasaidia maskini. 37 Hata hivyo aliugua akafa. Wakamwosha na kumlaza katika chumba cha ghorofani. 38 Kwa kuwa Jopa hapakuwa mbali sana na Lida, wanafunzi waliposikia kuwa Petro yuko Lida, waliwatuma wenzao wawili wakamwambie, “Tafadhali njoo huku pasipo kukawia.” 39 Kwa hiyo Petro akaharakisha akaenda nao Jopa. Alipowasili wakampeleka hadi kwenye chumba alipokuwa amelazwa marehemu Dor kasi. Wajane wengi walikuwa wamemzunguka marehemu wakilia na kuonyesha mavazi ambayo Dorkasi alikuwa amewashonea alipokuwa hai. 40 Petro akawatoa wote nje, kisha akapiga magoti akaomba; akaugeukia ule mwili akasema, “Tabita, Amka!” Dorkasi akafumbua macho na alipomwona Petro, akaketi. 41 Petro akamshika mkono akamsaidia kusimama. Ndipo alipowaita wale waamini na wajane aka wakabidhi Dorkasi akiwa hai. 42 Habari hizi zilienea sehemu zote za Jopa. Na watu wengi wakamwamini Bwana.

Read full chapter