18 Kesho yake Paulo alikwenda nasi kwa Yakobo, na wazee wote wa kanisa walikuwepo. 19 Baada ya kuwasalimu, Paulo alitoa taarifa kamili ya mambo yote ambayo Mungu alifanya kati ya watu wa mataifa kwa kumtumia yeye. 20 Baada ya maelezo yake wote walimtukuza Mungu. Ndipo wakamwambia, “Unavyoona ndugu, kuna maelfu ya Wayahudi walioamini; nao wote wanaishika sheria kwa bidii. 21 Lakini wamekuwa wakiambiwa habari zako kuwa wewe umew afundisha Wayahudi wanaoishi na watu wa mataifa waache kushika sheria za Musa; na kuwaambia wasitahiri watoto wao, au kufuata mila za Kiyahudi. 22 Sasa tufanyeje? Kwa maana watasikia kwamba umefika Yerusalemu. 23 Kwa hiyo fanya kama tunavyokushauri. Tunao watu wanne hapa ambao wameweka nadhiri. 24 Wachukue hawa ukajitakase pamoja nao na ulipe gharama zao ili wanyoe nywele zao. Kwa njia hii kila mtu atafahamu ya kuwa mambo waliyosikia si ya kweli na kwamba wewe unashika sheria. 25 Lakini wale watu wa mataifa walioamini tumewapelekea barua tukiwaambia kuwa tumeamua wajitenge na kitu cho chote ambacho kimetolewa kwanza kama sadaka kwa miungu ya sanamu na wasinywe damu au kula nyama ya mnyama aliyeuawa kwa kunyongwa. Tena ni lazima wajitenge na uasherati.” 26 Kwa hiyo Paulo akawachukua wale watu na kesho yake akajita kasa pamoja nao. Akaingia ndani ya Hekalu ili akatoe taarifa ya tarehe ambayo siku zao za utakaso zitamalizika na sadaka kutolewa kwa ajili ya kila mmoja wao.

Read full chapter