Add parallel Print Page Options

Kuja kwa Roho Mtakatifu

Siku ya Pentekoste ilipofika, wote walikuwa pamoja sehemu moja. Ghafla sauti ikaja kutoka mbinguni. Ilikuwa kama sauti ya upepo mkali unaovuma. Sauti hii ikajaa katika nyumba yote walimokuwa. Waliona miali iliyoonekana kama ndimi za moto. Miali ilitengana na kukaa juu ya kila mmoja wao pale. Wote walijaa Roho Mtakatifu na wakaanza kuzungumza kwa lugha tofauti. Roho Mtakatifu aliwapa uwezo wa kuzungumza lugha hizi.

Wakati haya yanatokea, walikuwepo Wayahudi waliorudi makwao. Hawa walikuwa wacha Mungu kutoka kila taifa ulimwenguni waliokuja mjini Yerusalemu. Kundi kubwa lilikusanyika kwa sababu walisikia kelele. Walishangaa kwa sababu, mitume walipokuwa wakitamka maneno kila mtu alisikia kwa lugha ya kwao.

Watu wote walilishangaa hili. Hawakuelewa ni kwa namna gani mitume waliweza kufanya hili. Wakaulizana, “Tazama! Watu wote hawa tunaowasikia wanatoka Galilaya.[a] Lakini tunawasikia wanatamka maneno kwa lugha zetu za asili. Hili linawezekanaje? Sisi tunatoka sehemu hizo mbalimbali: Parthia, Umedi, Elamu, Mesopotamia, Uyahudi, Kapadokia, Ponto, Asia, 10 Frigia, Pamfilia, Misri na maeneo ya Libya karibu na mji wa Kirene, Rumi, 11 Krete na Uarabuni. Baadhi yetu ni Wayahudi kwa kuzaliwa na wengine si Wayahudi, bali wamechagua kumwabudu Mungu kama Wayahudi. Tunatoka katika nchi hizi mbalimbali, lakini tunawasikia watu hawa wakizungumza kwa lugha zetu tofauti! Sisi sote tunaweza kuelewa yote wanayosema kuhusu matendo makuu ya Mungu.”

12 Watu wote walistaajabu na pia walichanganyikiwa. Wakaulizana, “Hii yote inamaanisha nini?” 13 Lakini wengine waliwacheka mitume, wakisema wamelewa kwa mvinyo mwingi waliokunywa.

Petro Azungumza na Watu

14 Ndipo Petro akasimama akiwa pamoja na mitume wengine kumi na moja. Akapaza sauti ili watu wote waweze kusikia. Alisema, “Ndugu zangu Wayahudi, nanyi nyote mnaoishi Yerusalemu. Nitawaeleza kuhusu jambo lililotokea, nisikilizeni kwa makini. 15 Watu hawa hawajalewa kwa mvinyo kama mnavyodhani; bado ni saa tatu asubuhi. 16 Lakini Nabii Yoeli aliandika kuhusu jambo hili mnaloliona likitokea hapa. Aliandika:

17 ‘Mungu anasema: Katika siku za mwisho,
    nitaimimina Roho yangu kwa watu wote.
Wana wenu na binti zenu watatabiri.
    Vijana wenu wataona maono,
    na wazee wenu wataota ndoto.
18 Katika siku hizo nitaimimina Roho
    yangu kwa watumishi wangu,
    wanaume na wanawake, nao watatabiri.
19 Nitafanya maajabu juu angani.
    Nitasababisha ishara chini duniani.
    Kutakuwa damu, moto na moshi mzito.
20 Jua litakuwa giza,
    na mwezi utakuwa mwekundu kama damu
    kabla ya ile siku kuu yenye utukufu ya Bwana kuja.
21 Na kila amwombaye Bwana’[b] ataokolewa.(A)

22 Ndugu zangu Waisraeli, sikilizeni ninayowaambia: Mungu aliwaonesha wazi kuwa Yesu kutoka Nazareti alikuwa mtu wake. Mungu alilithibitisha hili kwa miujiza, maajabu na ishara alizotenda Yesu. Ninyi nyote mliyaona mambo haya, na mnajua hii ni kweli. 23 Yesu aliletwa kwenu, nanyi mkamwua. Kwa kusaidiwa na watu wasioijali sheria yetu, mlimpigilia msalabani. Lakini Mungu alijua hili lingetokea. Ulikuwa mpango wake, mpango alioutengeneza tangu mwanzo. 24 Yesu aliteseka kwa maumivu makali ya kifo, lakini Mungu alimweka huru. Akamfufua kutoka kwa wafu. Mauti ilishindwa kumshikilia. 25 Daudi alilisema hili kuhusu Yesu:

‘Sijasahau kuwa Bwana yu pamoja nami.
    Yupo hapa pembeni yangu,
    hivyo hakuna kinachoweza kunidhuru.
26 Ndiyo sababu ninafurahi sana,
    na ninaimba kwa furaha!
    Lipo tumaini hata kwa ajili ya mwili wangu huu dhaifu,
27 kwa sababu wewe Bwana hutaniacha kaburini.[c]
    Hautauacha mwili wa mtumishi wako mwaminifu[d] kuozea huko.
28 Umenionyesha njia iendayo uzimani.
    Kuwa pamoja nawe kutanijaza furaha.’(B)

29 Ndugu zangu, ninaweza kuwaambia kwa ujasiri kuhusu Daudi, baba yetu mkuu. Alikufa, akazikwa, na kaburi lake liko hapa pamoja nasi hata leo. 30 Alikuwa nabii na alijua kitu ambacho Mungu alisema. Mungu alimwahidi Daudi kwa kuweka Agano kuwa mzaliwa katika familia yake mwenyewe ataketi kwenye kiti cha enzi cha Daudi kama mfalme.[e] 31 Daudi aliliona hili kabla halijatokea. Ndiyo maana alisema hivi kuhusu mfalme ajaye:

‘Hakuachwa kaburini.
    Mwili wake haukuozea humo.’[f]

Daudi alizungumza kuhusu Masihi kufufuka kutoka kwa wafu.

Read full chapter

Footnotes

  1. 2:7 wanatoka Galilaya Watu walidhani kuwa watu wanaotoka Galilaya walikuwa wanaweza kuzungumza lugha yao tu.
  2. 2:21 kila amwombaye Bwana Kwa maana ya kawaida, “kila aliitiaye jina la Bwana”.
  3. 2:27 kaburini Kwa maana ya kawaida, “Kuzimu”. Pia katika mstari wa 31.
  4. 2:27 mtumishi wako mwaminifu Au “Mtakatifu wako”, kwa kawaida neno hili linamaanisha mtu aliyejitoa na kumpendeza Mungu.
  5. 2:30 Mungu alimwahidi … kama mfalme Tazama 2 Sam 7:12,13 na Zab 132:11.
  6. 2:31 Tazama Zab 16:10.