Kushuka Kwa Roho Mtakatifu

Ilipofika siku ya Pentekoste, waamini wote walikuwa wameku tana mahali pamoja. Ghafla, sauti kama mvumo mkubwa wa upepo uliwashukia kutoka mbinguni, ukaijaza nyumba yote walimokuwa wamekaa. Pakatokea kitu kama ndimi za moto ambao uligawanyika ukakaa juu ya kila mmoja wao. Wote walijazwa Roho Mtakatifu wakaamza kusema kwa lugha nyingine, kama Roho alivyowajalia kusema.

Wakati huo walikuwepo Yerusalemu Wayahudi wanaomcha Mungu kutoka nchi zote za dunia. Waliposikia kelele hizi, walikusany ika kwa wingi. Wote walishangaa kwa sababu waliwasikia waamini wakiongea lugha ya kila mmoja wao.

Wakastaajabu sana, wakasema, “Hawa wote wanaozungumza ni Wagalilaya. Imekuwaje basi tunawasikia wakinena lugha ya kila mmoja wetu? Hapa kuna Waparthi, Wamedi, Waelami, wakazi wa Mesopotamia, Yudea Kapadokia, Ponto na Asia, 10 Frigia, Pom filia, Misri na pande za Libya karibu na Kirene; na wageni kutoka Rumi, Wayahudi na watu walioingia dini ya Kiyahudi. 11 Watu wen gine wametoka Krete na Uarabuni. Sisi sote tunasikia watu hawa wakisema katika lugha zetu wenyewe mambo makuu ya ajabu aliyofa nya Mungu.” 12 Wakiwa wameshangaa wakaulizana, “Ni nini maana ya mambo haya?” 13 Lakini wengine waliwadhihaki wakasema, “Hawa wamelewa divai mpya!”

Mahubiri Ya Petro

14 Ndipo Petro akasimama na wale mitume kumi na mmoja, aka hutubia ule umati wa watu kwa sauti kuu akasema, “Wayahudi wen zangu na ninyi nyote mkaao Yerusalemu. Nisikilizeni kwa makini niwaambie jambo hili maana yake ni nini! 15 Hawa watu hawakulewa kama mnavyodhania, kwa maana sasa ni mapema mno, saa tatu asu buhi. 16 La, jambo hili lilitabiriwa na Nabii Yoeli aliposema, 17 ‘Mungu alisema, siku za mwisho nitawamiminia binadamu wote Roho yangu: wavulana wenu na binti zenu watatabiri, vijana wenu wataona maono na wazee wataota ndoto. 18 Ndio, hata watumishi wangu wa kiume na wa kike nitawamiminia Roho yangu, nao watata biri. 19 Nami nitafanya maajabu angani, na duniani nitaonyesha ishara, damu na moto na moshi mnene. 20 Jua litageuka kuwa giza na mwezi utakuwa mwekundu kama damu, kabla ya siku ya Bwana kuwa dia, siku ambayo itakuwa ya kutisha. 21 Lakini ye yote ata kayetubu na kukiri jina la Bwana, ataokoka.’

22 “Nawasihi ninyi Waisraeli mnisikilize. Yesu wa Nazareti alikuwa mtu aliyethibitishwa kwenu na Mungu kwa njia ya miujiza, maajabu na ishara, kama ninyi wenyewe mjuavyo. 23 Huyu Yesu ali tiwa mikononi mwenu kwa mpango na makusudi ya Mungu aliyoyafahamu tangu awali. Nanyi mlimwua kwa kumtundika na kumpigilia misumari msalabani, mkisaidiwa na watu waovu. 24 Lakini Mungu alimfufua kutoka kwa wafu akamwondolea uchungu wa mauti, kwa sababu hata kifo kisingaliweza kumzuia. 25 Daudi alisema hivi juu yake, ‘Nilimwona Bwana akiwa mbele yangu wakati wote, Bwana yuko upande wangu wa kulia ili nisiogope. 26 Kwa hiyo moyo wangu unafurahi na ulimi wangu unashangilia; mwili wangu nao una matumaini ya uzima. 27 Kwa maana wewe Bwana hutaniacha kuzimu; wala hutaacha mtakatifu wako ateseke na kuoza. 28 Wewe umenionyesha njia inifikishayo uzimani. Na uwepo wako ukiwepo nami nitajawa na furaha.’

29 “Ndugu zangu, nataka niwaambie wazi kwamba mfalme Daudi alikufa na kuzikwa, na kaburi lake lipo hata leo. 30 Lakini ali kuwa nabii, na alijua ya kuwa Mungu aliahidi kwa kiapo kwamba angempa mmoja wa uzao wake kiti chake cha ufalme. 31 Kwa hiyo Daudi akaona mambo ambayo yangetokea, akatamka juu ya kufufuka kwa Kristo, kwamba asingeachwa kuzimu, wala mwili wake usingehar ibiwa kwa kuoza.

Read full chapter

Kuja kwa Roho Mtakatifu

Siku ya Pentekoste ilipofika, wote walikuwa pamoja sehemu moja. Ghafla sauti ikaja kutoka mbinguni. Ilikuwa kama sauti ya upepo mkali unaovuma. Sauti hii ikajaa katika nyumba yote walimokuwa. Waliona miali iliyoonekana kama ndimi za moto. Miali ilitengana na kukaa juu ya kila mmoja wao pale. Wote walijaa Roho Mtakatifu na wakaanza kuzungumza kwa lugha tofauti. Roho Mtakatifu aliwapa uwezo wa kuzungumza lugha hizi.

Wakati haya yanatokea, walikuwepo Wayahudi waliorudi makwao. Hawa walikuwa wacha Mungu kutoka kila taifa ulimwenguni waliokuja mjini Yerusalemu. Kundi kubwa lilikusanyika kwa sababu walisikia kelele. Walishangaa kwa sababu, mitume walipokuwa wakitamka maneno kila mtu alisikia kwa lugha ya kwao.

Watu wote walilishangaa hili. Hawakuelewa ni kwa namna gani mitume waliweza kufanya hili. Wakaulizana, “Tazama! Watu wote hawa tunaowasikia wanatoka Galilaya.[a] Lakini tunawasikia wanatamka maneno kwa lugha zetu za asili. Hili linawezekanaje? Sisi tunatoka sehemu hizo mbalimbali: Parthia, Umedi, Elamu, Mesopotamia, Uyahudi, Kapadokia, Ponto, Asia, 10 Frigia, Pamfilia, Misri na maeneo ya Libya karibu na mji wa Kirene, Rumi, 11 Krete na Uarabuni. Baadhi yetu ni Wayahudi kwa kuzaliwa na wengine si Wayahudi, bali wamechagua kumwabudu Mungu kama Wayahudi. Tunatoka katika nchi hizi mbalimbali, lakini tunawasikia watu hawa wakizungumza kwa lugha zetu tofauti! Sisi sote tunaweza kuelewa yote wanayosema kuhusu matendo makuu ya Mungu.”

12 Watu wote walistaajabu na pia walichanganyikiwa. Wakaulizana, “Hii yote inamaanisha nini?” 13 Lakini wengine waliwacheka mitume, wakisema wamelewa kwa mvinyo mwingi waliokunywa.

Petro Azungumza na Watu

14 Ndipo Petro akasimama akiwa pamoja na mitume wengine kumi na moja. Akapaza sauti ili watu wote waweze kusikia. Alisema, “Ndugu zangu Wayahudi, nanyi nyote mnaoishi Yerusalemu. Nitawaeleza kuhusu jambo lililotokea, nisikilizeni kwa makini. 15 Watu hawa hawajalewa kwa mvinyo kama mnavyodhani; bado ni saa tatu asubuhi. 16 Lakini Nabii Yoeli aliandika kuhusu jambo hili mnaloliona likitokea hapa. Aliandika:

17 ‘Mungu anasema: Katika siku za mwisho,
    nitaimimina Roho yangu kwa watu wote.
Wana wenu na binti zenu watatabiri.
    Vijana wenu wataona maono,
    na wazee wenu wataota ndoto.
18 Katika siku hizo nitaimimina Roho
    yangu kwa watumishi wangu,
    wanaume na wanawake, nao watatabiri.
19 Nitafanya maajabu juu angani.
    Nitasababisha ishara chini duniani.
    Kutakuwa damu, moto na moshi mzito.
20 Jua litakuwa giza,
    na mwezi utakuwa mwekundu kama damu
    kabla ya ile siku kuu yenye utukufu ya Bwana kuja.
21 Na kila amwombaye Bwana’[b] ataokolewa.(A)

22 Ndugu zangu Waisraeli, sikilizeni ninayowaambia: Mungu aliwaonesha wazi kuwa Yesu kutoka Nazareti alikuwa mtu wake. Mungu alilithibitisha hili kwa miujiza, maajabu na ishara alizotenda Yesu. Ninyi nyote mliyaona mambo haya, na mnajua hii ni kweli. 23 Yesu aliletwa kwenu, nanyi mkamwua. Kwa kusaidiwa na watu wasioijali sheria yetu, mlimpigilia msalabani. Lakini Mungu alijua hili lingetokea. Ulikuwa mpango wake, mpango alioutengeneza tangu mwanzo. 24 Yesu aliteseka kwa maumivu makali ya kifo, lakini Mungu alimweka huru. Akamfufua kutoka kwa wafu. Mauti ilishindwa kumshikilia. 25 Daudi alilisema hili kuhusu Yesu:

‘Sijasahau kuwa Bwana yu pamoja nami.
    Yupo hapa pembeni yangu,
    hivyo hakuna kinachoweza kunidhuru.
26 Ndiyo sababu ninafurahi sana,
    na ninaimba kwa furaha!
    Lipo tumaini hata kwa ajili ya mwili wangu huu dhaifu,
27 kwa sababu wewe Bwana hutaniacha kaburini.[c]
    Hautauacha mwili wa mtumishi wako mwaminifu[d] kuozea huko.
28 Umenionyesha njia iendayo uzimani.
    Kuwa pamoja nawe kutanijaza furaha.’(B)

29 Ndugu zangu, ninaweza kuwaambia kwa ujasiri kuhusu Daudi, baba yetu mkuu. Alikufa, akazikwa, na kaburi lake liko hapa pamoja nasi hata leo. 30 Alikuwa nabii na alijua kitu ambacho Mungu alisema. Mungu alimwahidi Daudi kwa kuweka Agano kuwa mzaliwa katika familia yake mwenyewe ataketi kwenye kiti cha enzi cha Daudi kama mfalme.[e] 31 Daudi aliliona hili kabla halijatokea. Ndiyo maana alisema hivi kuhusu mfalme ajaye:

‘Hakuachwa kaburini.
    Mwili wake haukuozea humo.’[f]

Daudi alizungumza kuhusu Masihi kufufuka kutoka kwa wafu.

Read full chapter

Footnotes

  1. 2:7 wanatoka Galilaya Watu walidhani kuwa watu wanaotoka Galilaya walikuwa wanaweza kuzungumza lugha yao tu.
  2. 2:21 kila amwombaye Bwana Kwa maana ya kawaida, “kila aliitiaye jina la Bwana”.
  3. 2:27 kaburini Kwa maana ya kawaida, “Kuzimu”. Pia katika mstari wa 31.
  4. 2:27 mtumishi wako mwaminifu Au “Mtakatifu wako”, kwa kawaida neno hili linamaanisha mtu aliyejitoa na kumpendeza Mungu.
  5. 2:30 Mungu alimwahidi … kama mfalme Tazama 2 Sam 7:12,13 na Zab 132:11.
  6. 2:31 Tazama Zab 16:10.