42 Barnaba na Paulo walipokuwa wakitoka nje ya sinagogi watu waliwasihi warudi tena sabato ifuatayo wawaambie zaidi kuhusu mambo haya. 43 Baada ya mkutano wa sinagogi kumalizika Wayahudi wengi na waongofu wa dini ya Kiyahudi waliwafuata Paulo na Bar naba, nao wakazungumza na kuwahimiza wadumu katika neema ya Mungu. 44 Sabato iliyofuata karibu watu wote wa mji ule walikuja kusikiliza neno la Mungu. 45 Lakini Wayahudi walipoona lile kusanyiko kubwa la watu, waliona wivu, wakakanusha mafundisho ya Paulo na kumtukana. 46 Paulo na Barnaba wakazidi kufundisha kwa ujasiri, wakisema, “Ilikuwa ni lazima neno la Mungu lihubiriwe kwanza kwenu Wayahudi. Lakini kwa kuwa mnalikataa, mnajihukumu wenyewe kuwa hamstahili kupata uzima wa milele. Tutawahubiria watu wa mataifa mengine. 47 Kwa maana Bwana ametuagiza akisema, ‘Nimewaweka ninyi kuwa nuru kwa watu wa mataifa, ili mpeleke wokovu hadi pembe zote za dunia.”’ 48 Watu wa mataifa mengine waliposikia maneno haya walifurahi, wakalitukuza neno la Mungu; na wote waliochaguliwa kwa ajili ya uzima wa milele wakaamini. 49 Neno la Mungu likaenea sehemu zote katika jimbo lile. 50 Lakini Wayahudi waliwachochea wanawake waheshimiwa wamchao Mungu pamoja na viongozi maarufu wa mji, wakaanza kuwatesa Paulo na Barnaba na kisha wakawafukuza kutoka wilaya ile.

Read full chapter