Yesu Amponya Mtu Mwenye Pepo

Wakafika upande wa pili wa ziwa wakaingia katika jimbo la Wagerasi. Yesu alipotoka kwenye mashua, mtu mmoja mwenye pepo mchafu alitoka makaburini akaja kukutana naye. Mtu huyu aliishi makaburini wala hakuna aliyeweza kumfunga hata kwa minyororo , kwa maana mara nyingi alipofungwa kwa minyororo mikononi na vyuma miguuni, aliivunjavunja na hakuna mtu aliyekuwa na nguvu za kumshinda. Usiku na mchana alikaa makaburini na milimani aki piga makelele na kujikatakata kwa mawe.

Alipomwona Yesu kwa mbali, alimkimbilia akapiga magoti mbele yake, akapiga kelele kwa nguvu akasema, “Unataka nini kwangu, Yesu, Mwana wa Mungu Mkuu? Ninakusihi kwa jina la Mungu, usinitese!” Alisema hivi kwa kuwa Yesu alikuwa akimwambia, “Mtoke huyu mtu! Wewe pepo mchafu!”

Yesu akamwuliza, “Jina lako ni nani?” Akamjibu, “Jina langu ni jeshi, kwa maana tupo wengi.” 10 Akamwomba sana Yesu asiwapeleke nje ya jimbo lile. 11 Hapo hapo lilikuwapo kundi la nguruwe likilisha kando ya mlima. 12 Wale pepo wakamsihi Yesu, “Turuhusu tukawaingie wale nguruwe.” 13 Basi akawaruhusu. Wakamtoka yule mtu wakaenda wakawaingia wale nguruwe na kundi lote la nguruwe wapatao elfu mbili likatimka kasi kwenye mteremko ule, wakazama ziwani, wakafa.

14 Wale waliokuwa wakichunga hao nguruwe wakakimbilia mjini na vijijini kueleza yaliyotokea. Watu wakatoka kwenda kujionea mambo hayo.

15 Wakaja kwa Yesu, wakamwona yule mtu aliyekuwa amepagawa na pepo akiwa ameketi, amevaa nguo na pia akiwa na akili timamu. Wakaogopa. 16 Wale walioyaona mambo haya waliwaeleza wengine yaliyomto kea yule aliyekuwa na pepo na lile kundi la nguruwe. 17 Basi watu wakaanza kumwomba Yesu aondoke katika wilaya yao.

18 Yesu alipoanza kuingia kwenye mashua, yule mtu aliyekuwa amepagawa na pepo akamsihi Yesu waende pamoja. 19 Yesu akamka talia. Badala yake akamwambia, “Nenda nyumbani kwa jamaa yako ukawaeleze mambo makuu aliyokutendea Bwana na jinsi alivyokuhuru mia.” 20 Yule mtu akaenda akaanza kutangaza katika Dekapoli - yaani miji kumi, mambo makuu aliyomtendea Bwana. Na watu wote wakastaajabu.

Yesu Amponya Mama Aliyetokwa Damu

21 Yesu alipokwisha vuka tena na kufika ng’ambo ya pili, umati mkubwa wa watu ukamzunguka, yeye akiwa kando ya ziwa. 22 Kisha kiongozi mmoja wa sinagogi aliyeitwa Yairo akamjia Yesu akapiga magoti miguuni pake, 23 akamsihi, “Binti yangu mdogo ni mgonjwa mahututi. Tafadhali njoo umguse kwa mikono yako apate kupona na kuishi.” 24 Basi Yesu akaongozana naye. Umati mkubwa wa watu waliomfuata wakawa wanamsonga.

25 Na alikuwepo mama mmoja aliyekuwa amesumbuliwa na tatizo la kutokwa damu kwa miaka kumi na miwili. 26 Mama huyu alikuwa amehangaika sana, akiwa ametibiwa na waganga wa kila aina na kutumia fedha yake yote kwa waganga lakini hakupata nafuu. Hali yake ilizidi kuwa mbaya. 27 Alikuwa amesikia habari za Yesu kwa hiyo alimfuata kwa nyuma, akapenyeza kati ya watu, akaligusa vazi lake. 28 Maana alisema moyoni mwake, “Nikiligusa vazi lake tu, nitapona.” 29 Mara damu iliyokuwa inamtoka ikakauka; akajisikia amepona kabisa.

30 Yesu akafahamu kuwa nguvu zimemtoka. Akageuka, akawauliza wale watu, “Ni nani amenigusa?”

31 Wanafunzi wake wakamjibu, “Mbona unauliza ni nani ameku gusa? Huoni umati huu ulivyokusonga?” 32 Lakini Yesu alizidi kutazama aone ni nani aliyemgusa. 33 Kisha yule mwanamke, akijua kilichomtokea, akaja, akaanguka miguuni kwake akitetemeka kwa hofu, akamweleza ukweli wote. 34 Yesu akamwambia, “Binti, imani yako imekuponya. Nenda kwa amani, upone kabisa ugonjwa wako.”

Yesu Amfufua Binti Yairo

35 Alipokuwa akiongea, watu wakafika kutoka nyumbani kwa Yairo wakamwambia, “Usimsumbue tena mwalimu, binti yako amefar iki. ” 36 Lakini Yesu hakuyatilia maanani maneno hayo, akamwam bia Yairo, “Usiogope, bali amini tu.”

37 Hakumruhusu mtu mwingine amfuate isipokuwa Petro, Yakobo na Yohana, nduguye Yakobo.

38 Walipofika nyumbani kwa yule kiongozi wa sinagogi, Yesu aliona vurugu na watu wengi wakilia na kuomboleza kwa nguvu. 39 Alipoingia ndani, aliwaambia, “Kwa nini mnafanya vurugu na kuomboleza? Mtoto hakufariki bali amelala.” 40 Wale watu wakam cheka kwa dharau. Lakini yeye akawatoa wote nje, akawachukua baba na mama wa yule mtoto pamoja na wale wanafunzi aliokuwa nao, wakaenda pale alipokuwa yule mtoto. 41 Akamwinua mtoto akamwam bia, “Talitha kumi!” Maana yake, “Binti mdogo, nakwambia amka!’ ’

42 Mara yule mtoto akasimama, akaanza kutembea. Alikuwa na umri wa miaka kumi na miwili. Walipoona haya, walistaajabu sana. 43 Yesu akawaamuru wasimweleze mtu jambo hili, na akawaambia wampe yule mtoto chakula.

Yesu Amweka Huru Mtu Kutoka Pepo Wachafu

(Mt 8:28-34; Lk 8:26-39)

Wakafika ng'ambo ya ziwa, katika nchi walimoishi Wagerasi.[a] Yesu alipotoka katika mashua ile ghafla, mtu mmoja aliyekuwa na roho chafu alitoka makaburini kuja kumlaki. Mtu huyu aliishi makaburini, na hakuna mtu yeyote aliyeweza kumfunga hata kwa mnyororo, Watu walijaribu kila mara kumfunga kwa minyororo na vyuma kwenye miguu na mikono. Hata hivyo, aliweza kuivunja minyororo ile na pingu zile za vyuma wala hakuna aliyekuwa na nguvu za kutosha kumdhibiti. Kila mara usiku na mchana akiwa makaburini na kwenye milima alipiga kelele na kujikata kwa mawe.

Alipomwona Yesu kutoka mbali, alimkimbilia, na kusujudu mbele yake. Kisha akalia kwa sauti kubwa na kusema, “Unataka nini kwangu, Yesu Mwana wa Mungu Aliye Mkuu zaidi? Nakuomba uape mbele za Mungu kwamba hutanitesa.” Yule pepo alisema haya kwa sababu Yesu alikuwa anamwambia, “Mtoke huyo mtu, ewe pepo mchafu!”

Ndipo Yesu akamwuliza yule mtu, “Jina lako nani?”

Naye akamjibu, “Jina langu ni Jeshi,[b] kwa sababu tuko wengi.” 10 Yule pepo akamwomba Yesu tena na tena asiwaamuru kutoka katika eneo lile.

11 Kulikuwepo kundi kubwa la nguruwe likila katika kilima. 12 Wale pepo wakamwomba Yesu awatume waende katika lile kundi la nguruwe na kuliingia, 13 Naye akawaruhusu. Kwa hiyo pepo wachafu walimtoka mtu yule na kuwaingia nguruwe.[c] Kundi lile lilikuwa na idadi karibu ya elfu mbili, lilikimbia kuelekea kwenye kingo zenye mtelemko mkali na kutumbukia ziwani, ambamo walizama.

14 Wale waliowachunga walikimbia. Wakatoa taarifa mjini na katika maeneo jirani ya mashambani. Watu wakaja kuona ni kitu gani kilichotokea. 15 Watu hao wakamwendea Yesu. Nao wakamwona yule aliyekuwa na mashetani ameketi mahali pale, amevaa nguo na akiwa mwenye akili zake nzuri; huyu ni yule aliyekuwa amepagawa na jeshi la mashetani. Wakaogopa. 16 Wale waliokuwa wameona hili waliwasimulia kile kilichomtokea mtu yule aliyekuwa amepagawa na mashetani na kuhusu nguruwe wale. 17 Nao wakamwomba Yesu aondoke katika eneo lile.

18 Wakati Yesu akipanda katika mtumbwi, mtu yule aliyekuwa amepagawa na mashetani alimwomba Yesu afuatane naye. 19 Lakini Yesu hakumruhusu aende naye, isipokuwa alimwambia, “Nenda kwa watu wa kwenu, na uwaambie yote ambayo Bwana amekufanyia, na uwaambie jinsi alivyokuwa na huruma kwako.”

20 Hivyo mtu yule aliondoka, na akaanza kuwaeleza watu katika Dekapoli[d] mambo mengi ambayo Yesu amemtendea, na watu wote walistaajabu.

Yesu Anampa Uhai Msichana Aliyekufa na Kumponya Mwanamke Mgonjwa

(Mt 9:18-26; Lk 8:40-56)

21 Kisha, Yesu alivuka kurudi upande wa magharibi wa ziwa. Pale kundi kubwa la watu lilikusanyika kwake. Yeye alikuwa kando ya ziwa, na 22 mmoja wa viongozi wa sinagogi, aliyeitwa Yairo, alifika pale. Naye alipomwona Yesu, alipiga magoti miguuni pake. 23 Kisha akamwomba kwa msisitizo, akisema, “Binti yangu mdogo yu karibu kufa. Ninakuomba ufike na kumwekea mikono, ili kwamba apone na kuishi.”

24 Hivyo Yesu alienda pamoja naye. Na kundi kubwa la watu lilimfuata; nao walikuwa wakimsonga pande zote kumzunguka.

25 Alikuwepo mwanamke mmoja aliyekuwa akitoka damu (kama ilivyo desturi ya wanawake kila mwezi) kila siku kwa miaka kumi na miwili. 26 Huyu alikuwa ameteseka sana akiwa chini ya uangalizi wa madaktari wengi. Yeye alikuwa ametumia vyote alivyokuwa navyo. Hata hivyo hali yake iliendelea kuwa mbaya zaidi.

27 Wakati aliposikia juu ya Yesu, alimwendea kwa nyuma akiwa katika kundi lile na kuligusa joho lake. 28 Kwani alikuwa akijisemea mwenyewe, “Ikiwa nitagusa tu vazi lake, nitapona.” 29 Mara moja chanzo cha kutoka kwake damu kikakauka, na akajisikia mwilini mwake kwamba amepona matatizo yake. 30 Naye Yesu akatambua mara moja kwamba nguvu zilimtoka. Aligeuka nyuma na kuuliza “Nani aliyegusa mavazi yangu?”

31 Wanafunzi wake wakamwambia, “Uliliona kundi likisukumana kukuzunguka, nawe unauliza, Nani aliyenigusa?”

32 Lakini Yesu aliendelea kuangalia kumzunguka kuona ni nani aliyeyafanya haya. 33 Yule Mwanamke akiwa anatetemeka kwa hofu akijua nini kilichotokea kwake, alikuja na kuanguka mbele yake, akamweleza ukweli wote. 34 Kisha Yesu akamwambia, “Binti yangu imani yako imekuponya. Nenda kwa amani, na uendelee kupona matatizo yako.”

35 Wakati alipokuwa akizungumza haya watumishi walikuja kutoka nyumbani kwa afisa wa sinagogi. Nao wakamwambia yule afisa, “Binti yako amefariki kwa nini uendelee kumsumbua huyo mwalimu?”

36 Lakini Yesu aliyasikia yale waliyokuwa wakisema, na akamwaambia yule afisa wa sinagogi, “Usiogope. Amini tu.”

37 Naye hakumruhusu mtu yeyote kumfuata isipokuwa Petro, Yakobo na Yohana ndugu yake Yakobo, 38 nao wakaenda katika nyumba ya yule afisa wa sinagogi, na Yesu akaona vurugu na watu wakilia kwa sauti. 39 Yesu aliingia ndani na kuwaambia, “Za nini vurugu zote hizi na vilio hivi? Mtoto hajafa; amelala tu.” 40 Nao wakamcheka.

Yeye aliwatoa nje watu wote, akamchukua baba na mama wa mtoto na wale waliokuwa pamoja naye, akaenda hadi pale alipokuwepo mtoto, 41 akaushika mkono wa mtoto yule na kumwambia “Talitha koum!” (maana yake, “Msichana mdogo, ninakuambia amka usimame!”) 42 Yule msichana aliinuka mara moja na kuanza kutembea mahali pale. Naye alikuwa na miaka kumi na miwili. Nao mara moja wakaelemewa na mshangao mkubwa. 43 Yeye akawapa amri kuwa mtu yeyote asijue juu ya jambo hili. Kisha akawaambia wampatie msichana yule chakula ale.

Footnotes

  1. 5:1 Wagerasi Nakala zingine za Kiyunani zina “Wagadarini” na zingine zimewaita “Wagergesini”.
  2. 5:9 Jeshi Jina hili lina maana nyingi sana. Jina hili lina maana “wengi zaidi” Ni neno lililotumika kwa kundi la wanajeshi 6,000 wa Jeshi la Kirumi.
  3. 5:13 nguruwe Watu kijijini walikuwa wakiwatunza nguruwe katika kundi moja kubwa. Kundi hilo lilikuwa chanzo muhimu cha mapato kwa kijiji.
  4. 5:20 Dekapoli Eneo wanaloishi wasio Wayahudi mashariki mwa Galilaya inaloitwa pia Eneo la Miji Kumi.