20 Mnapokutana pamoja hamli chakula cha Bwana. 21 Kwa kuwa mnapokula, kila mmoja wenu anaendelea na chakula chake bila kun goja wengine, na mmoja anabaki na njaa wakati mwingine analewa. 22 Je, hamwezi mkala na kunywa kwenye nyumba zenu? Au mnadharau kanisa la Mungu na kuwafedhehesha wasio na kitu? Niwaambie nini?

Je, niwasifu juu ya jambo hili? La, sitawasifu!

23 Kwa maana mimi nilipokea kutoka kwa Bwana yale maagizo niliyowapa ninyi, kwamba Bwana Yesu, usiku ule aliposalitiwa, alitwaa mkate, 24 naye akiisha kushukuru , akaumega, akasema, “Huu ndio mwili wangu, ambao ni kwa ajili yenu. Fanyeni hivi kwa ukumbusho wangu.” 25 Na vivi hivi baada ya kula akakitwaa kikombe, akisema, “Hiki kikombe ni agano jipya katika damu yangu. Fanyeni hivi kila mnywapo kwa ukumbusho wangu.” 26 Maana kila mlapo mkate huu na kunywa katika kikombe hiki, mnatangaza kifo cha Bwana mpaka atakapokuja.

27 Kwa hiyo mtu ye yote anayekula mkate huo au kukinywea kikombe hicho isivyostahili, atakuwa na hatia juu ya mwili na damu ya Bwana. 28 Kila mtu ajichunguze mwenyewe, na ndipo aule mkate na kukinywea kikombe. 29 Kwa maana mtu ye yote alaye na kunywa pasipo kutambua mwili wa Bwana, anajiletea hukumu juu yake mwenyewe.

Read full chapter