Yohana 15
Neno: Bibilia Takatifu
Mzabibu Wa Kweli
15 ‘Mimi ni mzabibu wa kweli na Baba yangu ndiye mkulima. 2 Kila tawi ndani yangu lisilozaa matunda, Baba yangu hulikata; na kila tawi lizaalo, yeye hulisafisha ili lipate kuzaa matunda zaidi. 3 Ninyi mmekwisha kuwa safi kwa sababu ya mafundisho nili yowapa. 4 Kaeni ndani yangu nami nikae ndani yenu. Kama vile tawi lisivyoweza kuzaa matunda pasipo kuwa sehemu ya mzabibu, vivyo hivyo, ninyi msipokaa ndani yangu hamwezi kufanya lo lote. 5 Mimi ni mzabibu; ninyi ni matawi; anayekaa ndani yangu nami ndani yake, huyo huzaa matunda mengi sana; maana pasipo mimi ninyi hamwezi kufanya lo lote. 6 Mtu asipokaa ndani yangu hutupwa nje kama tawi na kunyauka. Matawi hayo hukusanywa na kutupwa motoni, yakateketea. 7 Ninyi mkikaa ndani yangu na maneno yangu yakikaa ndani yenu, ombeni lo lote mtakalo nanyi mtatendewa. 8 Mnapozaa matunda kwa wingi Baba yangu anatukuzwa, na hivyo mnadhihirisha kuwa ninyi ni wanafunzi wangu.
9 “Kama Baba alivyonipenda mimi, hivyo ndivyo mimi nilivy owapenda ninyi; dumuni katika pendo langu. 10 Mkizishika amri zangu mtakaa ndani ya pendo langu kama mimi nilivyozishika amri za Baba yangu na kukaa katika pendo lake.
11 “Nimewaambia haya kusudi furaha yangu iwe ndani yenu, nanyi mpate kuwa na furaha iliyokamilika.
12 “Amri yangu ni hii: pendaneni kama nilivyowapenda. 13 Hakuna mtu mwenye upendo unaozidi ule wa mtu anayejitoa afe kwa ajili ya rafiki zake. 14 Ninyi ni rafiki zangu ikiwa mtafa nya ninayowaagiza. 15 Siwaiti ninyi watumishi tena kwa sababu mtumishi haelewi shughuli za bwana wake; bali nimewaita rafiki, kwa maana mambo yote niliyoyasikia kutoka kwa Baba yangu nimewa fahamisha. 16 Hamkunichagua, bali mimi nimewachagua ninyi na nimewatuma mwende mkazae matunda, na matunda yenu yapate kudumu, ili lo lote mtakalomwomba Baba katika jina langu, awatimizie. 17 Hii ndio amri yangu: pendaneni.
18 “Kama ulimwengu ukiwachukia, fahamuni kwamba ulinichukia mimi kabla haujawachukia ninyi. 19 Kama mngekuwa watu wa ulim wengu huu, ulimwengu ungeliwapenda. Ulimwengu unawachukia kwa sababu ninyi si wa ulimwengu huu na mimi nimewachagua kutoka katika ulimwengu.
20 “Kumbukeni lile neno nililowaambia, ‘Hakuna mtumishi aliye mkuu kuliko bwana wake.’ Kama wamenitesa mimi na ninyi pia watawatesa; kama wamelishika neno langu na neno lenu watalishika pia. 21 Lakini yote haya watawatendea kwa ajili yangu kwa sababu hawamfahamu Baba yangu ambaye amenituma. 22 Kama sikuja na kusema nao wasingalikuwa na hatia. Lakini sasa hawana udhuru kwa dhambi zao. 23 Mtu ye yote anayenichukia mimi anamchukia na Baba yangu. 24 Kama nilikuwa sikuwafanyia miujiza ambayo haijapata kufanywa na mtu mwingine ye yote, wasingalikuwa na hatia ya dhambi. Lakini wameona miujiza hii na bado wakatuchukia mimi na Baba yangu. 25 “Hali hii imetokea kama ilivyoandikwa katika Sheria kwamba, ‘Walinichukia pasipo sababu.’ 26 Lakini atakapokuja yule Msaidizi nitakayewapelekea kutoka kwa Baba, yaani yule Roho wa kweli atokaye kwa Baba, yeye atanishuhudia mimi. 27 Na ninyi pia ni mashahidi wangu kwa maana tangu mwanzo mmekuwa pamoja nami.”
Copyright © 1989 by Biblica