Kutoka kwa Yakobo, mtumishi wa Mungu na wa Bwana Yesu Kristo. Kwa makabila kumi na mawili yaliyotawanyika ulimwenguni. Salamu:

Imani Na Hekima

Ndugu wapendwa, mnapopatwa na majaribu mbalimbali, yahesab uni kuwa ni furaha tupu. Kwa maana mnafahamu ya kuwa kujaribiwa kwa imani yenu hujenga ustahimilivu. Na ustahimilivu ukimaliza kazi yake mtakuwa wakamilifu pasipo kupungukiwa na cho chote.

Lakini kama mtu ye yote kati yenu akipungukiwa na hekima, basi na amwombe Mungu, ambaye huwapa watu wote kwa ukarimu pasipo kulaumu, naye atapewa. Lakini aombe kwa imani pasipo shaka yo yote; maana mwenye mashaka ni kama wimbi la bahari ambalo husu kumwa na upepo, likitupwa huku na huku. Mtu kama huyo asidhani atapata kitu cho chote kutoka kwa Bwana; kwa maana yeye ni mtu mwenye nia mbili asiyekuwa na msimamo katika jambo lo lote.

Umaskini Na Utajiri

Ndugu asiye na cheo afurahi kwa sababu Bwana amemtukuza; 10 na tajiri afurahi anaposhushwa kwa maana atatoweka kama ua la mwituni. 11 Maana jua huchomoza na kwa mionzi yake mikali hukausha mimea, na maua yake huanguka na uzuri wake hupotea. Vivyo hivyo tajiri naye atafifia akiwa katika shughuli zake.

Kujaribiwa

12 Amebarikiwa mtu ambaye anavumilia majaribu, kwa sababu akisha stahimili atapewa taji ya uzima ambayo Mungu amewaahidi wale wampendao. 13 Mtu akijaribiwa asiseme, “Ninajaribiwa na Mungu,” kwa maana Mungu hajaribiwi na uovu na yeye hamjaribu mtu ye yote. 14 Lakini kila mtu hujaribiwa anapovutwa na kudanganywa na tamaa yake mwenyewe. 15 Kisha tamaa hiyo ikisha chukua mimba, huzaa dhambi; na dhambi ikisha komaa, huzaa mauti.

16 Ndugu zangu wapendwa, msidanganywe. 17 Kila kipawa chema na kila zawadi kamilifu hutoka mbinguni, ikishuka kutoka kwa Baba wa nuru za mbinguni ambaye habadiliki kama kivuli. 18 Kwa kupenda kwake mwenyewe alituzaa kwa neno la kweli, kusudi tuwe kama mavuno ya kwanza katika viumbe vyake.

Kusikia Na Kutenda

19 Ndugu wapendwa, fahamuni jambo hili: kila mtu awe mwepesi wa kusikia, bali si mwepesi wa kusema wala kukasirika. 20 Maana hasira ya mwanadamu haitendi haki ya Mungu. 21 Kwa hiyo epukeni uchafu wote na uovu ambao umeenea, mkapokee kwa unyenyekevu lile neno lililopandwa mioyoni mwenu ambalo linaweza kuokoa nafsi zenu.

22 Basi muwe watendaji wa neno na wala msiwe wasikilizaji tu, ambao wanajidanganya wenyewe. 23 Kwa maana kama mtu ni msi kilizaji tu wa neno na wala hatekelezi alilosikia, atafanana na mtu ajitazamaye uso wake katika kioo, 24 na baada ya kujiona alivyo, huenda zake na mara moja husahau anavyofanana. 25 Lakini mtu anayeangalia kwa makini katika sheria kamilifu, ile sheria iletayo uhuru, na akaendelea kufanya hivyo bila kusahau alichosi kia, bali akakitekeleza, atabarikiwa katika kile anachofanya.

26 Mtu akidhani kuwa ana dini na huku hautawali ulimi wake, anajidanganya mwenyewe na dini yake ni bure. 27 Dini iliyo safi, isiyo na uchafu mbele za Mungu Baba, ndio hii: kuwasaidia yatima na wajane katika dhiki zao, na kujilinda mwenyewe usichafuliwe na ulimwengu.