Makao Ya Mbinguni

Kwa maana twajua kwamba kama hema hii tunamoishi tukiwa ulimwenguni itaharibiwa, tunalo jengo kutoka kwa Mungu, nyumba ya milele mbinguni, ambayo haikujengwa kwa mikono ya wanadamu. Maana sasa twaugua, tukitamani kuvikwa makao yetu ya mbinguni, kwa kuwa tukiisha kuvikwa hatutaonekana tena tukiwa uchi. Tukiwa bado tunaishi katika hema hii tunaugua na kulemewa, kwa maana hatutaki kukaa bila nguo bali tunatamani kuvikwa makao yetu ya mbinguni ili ile hali ya kufa imezwe na uhai. Mungu ndiye aliyetuandaa kwa shabaha hii, naye ametupa Roho wake kama mdha mana, kutuhakikishia mambo yajayo baadaye. Kwa hiyo wakati wote tuna ujasiri mkuu. Tunajua kwamba wakati tukiwa katika mwili huu, tuko mbali na nyumbani kwa Bwana. Tunaishi kwa imani na si kwa kuona. Nasema tuna ujasiri na ingekuwa afadhali kuuacha mwili huu tukaishi nyumbani na Bwana. Kwa hiyo, kama tuko nyumbani katika mwili huu au tuko mbali nao, lengo letu ni kumpendeza Bwana. 10 Kwa kuwa sisi sote inatubidi kusimama mbele ya kiti cha hukumu cha Kristo. Na kila mmoja atapokea mema au mabaya, kulingana na matendo yake alipokuwa katika mwili.

Huduma Ya Upatanisho

11 Kwa hiyo tukijua umuhimu wa kumcha Bwana tunajaribu kuwa vuta watu. Mungu anatufahamu fika. Tunaamini kwamba dhamiri zenu pia zinatufahamu tulivyo. 12 Hatujaribu kujipendekeza kwenu tena, lakini tunataka kuwapeni nafasi mjisifu juu yetu ili muweze kuwajibu hao wanaojisifia mambo yanayoonekana badala ya mambo yaliyo moyoni. 13 Kama tumeehuka, ni kwa ajili ya Mungu; lakini kama tuna akili timamu ni kwa faida yenu. 14 Kwa kuwa upendo wa Kristo unatusukuma, tunaamini ya kuwa mmoja alikufa kwa ajili ya wote kwa hiyo wote walikufa. 15 Naye alikufa kwa ajili ya watu wote ili wote wanaoishi, wasiishi tena kwa ajili yao wenyewe, bali kwa ajili yake yeye aliyekufa na kufufuka tena kwa ajili yao.

16 Tangu sasa hatumtazami mtu ye yote namna ya kibinadamu, ingawaje hapo mwanzo tulimtazama Kristo kwa namna ya kibinadamu. Hatumtazami hivyo tena. 17 Kwa hiyo mtu akiwa ndani ya Kristo, amekuwa kiumbe kipya; ya kale yamepita, tazama, mapya yamekuja. 18 Haya yote yanatoka kwa Mungu, ambaye kwa njia ya Yesu Kristo ametupatanisha na mwenyewe, na akatupa huduma ya upatanisho. 19 Ndani ya Kristo Mungu aliupatanisha ulimwengu na yeye mwe nyewe, asiwahesabie watu dhambi zao. Naye ametukabidhi ujumbe huu wa upatanisho.

20 Kwa hiyo sisi ni mabalozi wa Kristo, Mungu anatutumia sisi kuwasihi ninyi. Na sisi tunawasihi ninyi kwa niaba ya Kristo: mpatanishwe na Mungu. 21 Mungu alimfanya yeye ambaye hakujua dhambi, awe dhambi kwa ajili yetu ili ndani yake tupate kuwa haki ya Mungu.