Maisha Yanayompendeza Mungu

Hatimaye, ndugu wapendwa, tuliwaelekeza namna mnavyopaswa kuishi ili kumpendeza Mungu. Na kweli ndivyo mnavyoishi. Sasa tunawaombeni na kuwasihi katika jina la Bwana Yesu, mwendelee kufanya hivyo zaidi na zaidi. Mnafahamu maelekezo tuliyowapa kwa mamlaka ya Bwana Yesu.

Mungu anapenda ninyi muwe watakatifu, mjiepushe na maisha ya zinaa; na kwamba kila mmoja wenu ajifunze kuishi na mke wake mwenyewe kwa njia ya utakatifu na heshima; si kwa kutawaliwa na tamaa mbaya kama watu wa mataifa wasiomjua Mungu. Katika jambo hili mtu asije akamkosea au kumdanganya ndugu yake. Kama tulivy okwisha kuwaambia na kuwaonya, Bwana atawaadhibu watu watendao dhambi zote za aina hii. Kwa maana Mungu hakutuita tutawaliwe na mawazo machafu, bali tuishi maisha ya utakatifu. Kwa hiyo mtu ye yote anayekataa mafundisho haya hamkatai mwanadamu bali anamkataa Mungu anayewapa ninyi Roho wake Mtakatifu.

Hatuna haja ya kuwaandikia kuhusu upendo kati ya ndugu, kwa maana ninyi wenyewe mmekwisha kufundishwa na Mungu mpendane ninyi kwa ninyi 10 na kwa kweli mnawapenda ndugu wote wa Makedonia yote. Hata hivyo, ndugu zetu, tunawasihi mwendelee kuwapenda zaidi sana. 11 Jitahidini kuishi maisha ya utulivu, kila mtu akishughulikia mambo yake mwenyewe na kufanya kazi kwa mikono yenu, kama tulivyowaambia. 12 Kwa njia hii maisha yenu ya kila siku yatawaletea sifa kutoka kwa watu wasioamini na wala hamtahi taji kuwategemea watu wengine.

Kufufuliwa Kwa Wafu Na Kuja Kwa Bwana

13 Ndugu wapendwa, hatupendi mkose kujua kuhusu wale wanaokufa, au mhuzunike kama watu wasiokuwa na tumaini. 14 Tunaamini kwamba Yesu alikufa na kufufuka, kwa hiyo tunaamini kwamba Mungu atawainua wale waliokufa pamoja na Kristo wakiwa ndani yake. 15 Kama alivyosema Bwana mwenyewe, tunawaambieni kuwa sisi ambao tuko hai bado, tutakaokuwa hai mpaka Bwana arudi, kwa hakika hatutawatangulia wale waliokwisha kufa.

16 Kwa maana Bwana mwenyewe atashuka toka mbinguni, akitoa amri kwa sauti kuu pamoja na sauti ya malaika mkuu na sauti ya tarumbeta ya Mungu; na wale waliokufa wakiwa wanamwamini Kristo watafufuka kwanza. 17 Kisha sisi tulio hai bado, tuliosalia, tutanyakuliwa pamoja nao katika mawingu tukutane na Bwana angani. Na hivyo tutakuwa na Bwana milele. 18 Kwa hiyo farijianeni kwa maneno haya.