Yesu Amponya Mvulana Mwenye Pepo

14 Walipowafikia wale wanafunzi wengine, waliwakuta wame zungukwa na umati mkubwa wa watu na baadhi ya walimu wa sheria wakibishana nao. 15 Mara wale watu walipomwona Yesu, walistaaj abu sana, wakamkimbilia, wakamsalimu. 16 Akawauliza wanafunzi wake, “Mnabishana nini nao?”

17 Mtu mmoja katika ule umati wa watu akajibu, “Mwalimu, nimemleta kwako mtoto wangu wa kiume kwa maana amepagawa na pepo ambaye amemfanya kuwa bubu. 18 Kila mara pepo huyo amwingiapo mwanangu, humwangusha chini na kumfanya atokwe povu mdomoni na kusaga meno, kisha mwili wake hukauka. Nimewaomba wanafunzi wako wamtoe pepo huyo, lakini hawakuweza.”

19 Yesu akawaambia, “Ninyi kizazi kisicho na imani! Nita kuwa nanyi mpaka lini? Nitawavumilia mpaka lini? Mleteni huyo mtoto kwangu!” 20 Wakamleta. Yule pepo alipomwona Yesu, alimtia yule mvulana kifafa, akaanguka chini akajiviringisha viringisha huku akitokwa na povu mdomoni. 21 Yesu akamwuliza baba yake, “Mwanao amekuwa na hali hii tangu lini?” Akamjibu, “Tangu utoto wake. 22 Na mara nyingi huyo pepo amemwangusha kwenye moto au kwenye maji ili kuangamiza maisha yake. Lakini kama wewe unaweza kufanya cho chote, tafadhali tuonee huruma, utusaidie.” 23 Yesu akasema, “Kama unaweza! Kila kitu kinawezekana kwa mtu mwenye imani.” 24 Ndipo yule baba akasema kwa sauti, “Ninaamini. Nisaidie niweze kuamini zaidi!” 25 Naye Yesu ali poona umati wa watu unazidi kusongana kuja hapo walipokuwa, akam kemea yule pepo mchafu akisema, “Wewe pepo bubu na kiziwi, naku amuru umtoke, usimwingie tena!” 26 Yule pepo akapiga kelele, akamtia kifafa kwa nguvu kisha akatoka. Yule mvulana alionekana kama amekufa; kwa hiyo watu wengi wakasema, “Amekufa.” 27 Lakini Yesu akamshika mkono akamwinua, naye akasimama.

28 Walipokwisha kuingia ndani ya nyumba, wanafunzi wake wakamwuliza wakiwa peke yao, “Mbona sisi hatukuweza kumtoa huyo pepo?” 29 Yesu akawajibu, “Pepo wa aina hii hawezi kutoka isi pokuwa kwa maombi.”

Read full chapter