Yesu Amponya Mtu Mwenye Pepo

Wakafika upande wa pili wa ziwa wakaingia katika jimbo la Wagerasi. Yesu alipotoka kwenye mashua, mtu mmoja mwenye pepo mchafu alitoka makaburini akaja kukutana naye. Mtu huyu aliishi makaburini wala hakuna aliyeweza kumfunga hata kwa minyororo , kwa maana mara nyingi alipofungwa kwa minyororo mikononi na vyuma miguuni, aliivunjavunja na hakuna mtu aliyekuwa na nguvu za kumshinda. Usiku na mchana alikaa makaburini na milimani aki piga makelele na kujikatakata kwa mawe.

Alipomwona Yesu kwa mbali, alimkimbilia akapiga magoti mbele yake, akapiga kelele kwa nguvu akasema, “Unataka nini kwangu, Yesu, Mwana wa Mungu Mkuu? Ninakusihi kwa jina la Mungu, usinitese!” Alisema hivi kwa kuwa Yesu alikuwa akimwambia, “Mtoke huyu mtu! Wewe pepo mchafu!”

Yesu akamwuliza, “Jina lako ni nani?” Akamjibu, “Jina langu ni jeshi, kwa maana tupo wengi.” 10 Akamwomba sana Yesu asiwapeleke nje ya jimbo lile. 11 Hapo hapo lilikuwapo kundi la nguruwe likilisha kando ya mlima. 12 Wale pepo wakamsihi Yesu, “Turuhusu tukawaingie wale nguruwe.” 13 Basi akawaruhusu. Wakamtoka yule mtu wakaenda wakawaingia wale nguruwe na kundi lote la nguruwe wapatao elfu mbili likatimka kasi kwenye mteremko ule, wakazama ziwani, wakafa.

14 Wale waliokuwa wakichunga hao nguruwe wakakimbilia mjini na vijijini kueleza yaliyotokea. Watu wakatoka kwenda kujionea mambo hayo.

15 Wakaja kwa Yesu, wakamwona yule mtu aliyekuwa amepagawa na pepo akiwa ameketi, amevaa nguo na pia akiwa na akili timamu. Wakaogopa. 16 Wale walioyaona mambo haya waliwaeleza wengine yaliyomto kea yule aliyekuwa na pepo na lile kundi la nguruwe. 17 Basi watu wakaanza kumwomba Yesu aondoke katika wilaya yao.

18 Yesu alipoanza kuingia kwenye mashua, yule mtu aliyekuwa amepagawa na pepo akamsihi Yesu waende pamoja. 19 Yesu akamka talia. Badala yake akamwambia, “Nenda nyumbani kwa jamaa yako ukawaeleze mambo makuu aliyokutendea Bwana na jinsi alivyokuhuru mia.” 20 Yule mtu akaenda akaanza kutangaza katika Dekapoli - yaani miji kumi, mambo makuu aliyomtendea Bwana. Na watu wote wakastaajabu.

Yesu Amponya Mama Aliyetokwa Damu

21 Yesu alipokwisha vuka tena na kufika ng’ambo ya pili, umati mkubwa wa watu ukamzunguka, yeye akiwa kando ya ziwa. 22 Kisha kiongozi mmoja wa sinagogi aliyeitwa Yairo akamjia Yesu akapiga magoti miguuni pake, 23 akamsihi, “Binti yangu mdogo ni mgonjwa mahututi. Tafadhali njoo umguse kwa mikono yako apate kupona na kuishi.” 24 Basi Yesu akaongozana naye. Umati mkubwa wa watu waliomfuata wakawa wanamsonga.

25 Na alikuwepo mama mmoja aliyekuwa amesumbuliwa na tatizo la kutokwa damu kwa miaka kumi na miwili. 26 Mama huyu alikuwa amehangaika sana, akiwa ametibiwa na waganga wa kila aina na kutumia fedha yake yote kwa waganga lakini hakupata nafuu. Hali yake ilizidi kuwa mbaya. 27 Alikuwa amesikia habari za Yesu kwa hiyo alimfuata kwa nyuma, akapenyeza kati ya watu, akaligusa vazi lake. 28 Maana alisema moyoni mwake, “Nikiligusa vazi lake tu, nitapona.” 29 Mara damu iliyokuwa inamtoka ikakauka; akajisikia amepona kabisa.

30 Yesu akafahamu kuwa nguvu zimemtoka. Akageuka, akawauliza wale watu, “Ni nani amenigusa?”

31 Wanafunzi wake wakamjibu, “Mbona unauliza ni nani ameku gusa? Huoni umati huu ulivyokusonga?” 32 Lakini Yesu alizidi kutazama aone ni nani aliyemgusa. 33 Kisha yule mwanamke, akijua kilichomtokea, akaja, akaanguka miguuni kwake akitetemeka kwa hofu, akamweleza ukweli wote. 34 Yesu akamwambia, “Binti, imani yako imekuponya. Nenda kwa amani, upone kabisa ugonjwa wako.”

Yesu Amfufua Binti Yairo

35 Alipokuwa akiongea, watu wakafika kutoka nyumbani kwa Yairo wakamwambia, “Usimsumbue tena mwalimu, binti yako amefar iki. ” 36 Lakini Yesu hakuyatilia maanani maneno hayo, akamwam bia Yairo, “Usiogope, bali amini tu.”

37 Hakumruhusu mtu mwingine amfuate isipokuwa Petro, Yakobo na Yohana, nduguye Yakobo.

38 Walipofika nyumbani kwa yule kiongozi wa sinagogi, Yesu aliona vurugu na watu wengi wakilia na kuomboleza kwa nguvu. 39 Alipoingia ndani, aliwaambia, “Kwa nini mnafanya vurugu na kuomboleza? Mtoto hakufariki bali amelala.” 40 Wale watu wakam cheka kwa dharau. Lakini yeye akawatoa wote nje, akawachukua baba na mama wa yule mtoto pamoja na wale wanafunzi aliokuwa nao, wakaenda pale alipokuwa yule mtoto. 41 Akamwinua mtoto akamwam bia, “Talitha kumi!” Maana yake, “Binti mdogo, nakwambia amka!’ ’

42 Mara yule mtoto akasimama, akaanza kutembea. Alikuwa na umri wa miaka kumi na miwili. Walipoona haya, walistaajabu sana. 43 Yesu akawaamuru wasimweleze mtu jambo hili, na akawaambia wampe yule mtoto chakula.